WAIFANYA NDIO NJIA YA KUPITIA KILAAINI
Nidhahiri kwamba Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere
(JNIA), sasa ni kitovu cha kusafirisha dawa za kulevya nje ya nchi. Katika
kipindi cha takribani wiki mbili tu, Watanzania wanne wamekamatwa
ughaibuni wakiwa na shehena ya dawa hizo ambazo walisafirisha kutoa
Tanzania kwenda nje kupitia uwanja huo bila ya kukamatwa. Mara
ya kwanza walikuwa ni wasichana wawili, Agnes Jerald (25) na Melisa
Edward (24), ambao walikamatwa Afrika Kusini na kushtakiwa nchini humo. Walikamatwa
Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo wakiwa na shehena ya kilo
150 ya dawa aina ya Crystal Methamphetamine zenye thamani ya zaidi ya
Sh. bilioni 6.8. Wasichana hao walikamatwa Julai 5, mwaka huu baada ya
kuwasili Johannesburg wakitokea Tanzania wakisafiri kwa ndege ya Shirika
la Ndege la Afrika Kusini (SAA) na walikamatwa na Maofisa wa Mamlaka ya
Mapato ya nchi hiyo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver
Tambo, uliopo eneo la Kempton Park.
Ijumaa wiki hii, Watanzania wengine wawili, walikamatwa Hong Kong
wakiwa na dawa za kulevya aina ya cocaine na heroine zenye thamani ya
bilioni 7.6 akiwamo mmoja aliyekamatwa akitokea Dar es Salaam kupitia
Dubai hadi Honh Kong. Matukio
haya yote yanatokea wakati wakuu wa Uwanja wa ndege wa Julius Nyerere
zinakopitishwa wakiwa hawana cha kusema juu ya uharamia huo unaotokea
kwenye kitovu cha mawasiliano cha nchi.Jana,
Kamanda wa Polisi Kikosi cha Viwanja vya Ndege Nchini, Deusdedit Kato,
alisema jalada la upelelezi kuhusu tukio la kukamatwa kwa wasichana
Afrika Kusini litapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) leo ingawa
hakuwa tayari kutaja watuhumiwa ni nani hasa wanaoshirikiana na
wafanyabiashara ya dawa hizo.
Kato alisema hawezi kutaja majina ya watu waliobainika kwa sababu
kilichofanyika ni uchunguzi tu na kwamba DDP ndiye mwenye mamlaka ya
kuamua juu ya uchunguzi huo. “Siwezi kukuambia ni nini kimepatikana
katika uchunguzi wala kutaja majina ya watu, kwa kuwa mimi ninapeleka
nilichokichunguza kwa sababu naweza kukuambia lakini ikawa sio hivyo
kwani huu ni uchunguzi tu,” alisema. Aliongeza: “Naweza kupeleka jalada
langu la uchunguzi kwa DDP lakini kutokana na utalaam wake akagundua
kuna mapungufu, hapo tayari nitakuwa nimepotosha umma. Lakini pia akiona
upelelezi unajitosheleza yeye ndiye anaweza kuamua kupeleka
Mahakamani.” Kuhusu taarifa za kukamatwa kwa Watanzania wengine na dawa
za kulevya Julai 26, mwaka huu huko huko mjini Hong Kong, Kato alisema
bado wanafanya jitahada za kupata kwa undani taarifa hizo.
“Na mimi nimesikia, lakini hatujapata taarifa zaidi ili kujua
majina yao na kama kweli ni Watanzania. Inakuwa ngumu kupata taarifa kwa
sababu aina ya mawasiliano wanayotumia hawa Polisi wa Kimataifa
(Interpol ) ni tofauti na ya kwetu kwa hiyo tunategemea wao ndiyo watupe
taarifa,” alisema Kato. Naye Waziri wa Uchunguzi, Dk. Harrison
Mwanyembe, ambaye amejipatia sifa za utendaji katika siku za hivi
karibuni, kwa kuendesha timua timua katika taasisi zinazosimamiwa na
wizara yake kwa tuhuma za uzembe, amekuwa kimya na pengine kukwepa
kabisa kutia mguu katika sakata la dawa za kulevya JNIA. Wiki iliyopita
NIPASHE lilimtafuta Dk. Mwakyembe mwenye dhamana ya Viwanja vya Ndege
nchini kujua ni hatua gani amechukua, lakini alijibu kwamba hana taarifa
za kina kuhusu sakata hilo.
Uharamia huo wa dawa za kulevya umempa pia kigugumizi Mkurugenzi
wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Kamishna Robert Manumba, ambaye
amekwepa kuzungumzia sakata hilo na kusema liko kwa Kamanda wa Polisi,
Kitengo cha Kuzuia na Kupambana na Dawa za Kulevya, Geofrey
Nzowa. Kamanda Nzowa alipoulizwa alisema upelelezi bado unaendaelea
kubaini mambo mbalimbali yaliyoko nyuma ya tukio hilo. Alipoulizwa
ikiwa Polisi wamebaini mmiliki pamoja na maofisa walioruhusu kupitishwa
kwa dawa, Nzowa alisema uchunguzi unaangalia mambo mengi na ndiyo huo
utakuja na taarifa kamili. Taarifa kutoka Hong Kong za Ijumaa wiki
iliyopita zinaeleza kwamba, maofisa ushuru wa Uwanja wa Ndege wa Hong
Kong (HKIA), walimkamata kijana mmoja mwenye umri wa miaka 26 akitokea
Tanzania na alikuwa na dawa za kulevya aina ya heroin kilo 1.6 zenye
thamani ya Sh. bilioni 1.5, kwenye mzigo wake wa mkononi.
Taarifa zilieleza kwamba baadaye jioni siku hiyo hiyo, maofisa
hao walimkamata Mtanzania mwingine mwenye miaka 45 ambaye alipelekwa
hospitali na kutolewa gramu 240 za dawa za kulevya aina ya
heroin. Taarifa zaidi zilieleza kuwa Mtanzania mwingine mwenye miaka 28
alikamatwa akiwa na kilo 2.03 za cocaine. Takwimu zinaonyesha kumekuwa
na wimbi kubwa la Watanzania wanaojiingiza katika biashara haramu ya
dawa za kulevya ndani na nje ya nchi na kwamba, katika kipindi cha miaka
mitano iliyopita, watuhumiwa 10,799 walikamatwa kwa kujihusisha na
uharamia huo. Katika kipindi hicho, Watanzania 240 walikamatwa katika
nchi za Brazil, Pakistan na Afrika Kusini, na kuharibu taswira ya nchi
na kusababisha Watanzania wasio na hatia kupata usumbufu na masharti
magumu wanapotaka kusafiri kwenda nchi mbalimbali duniani.
No comments:
Post a Comment