Mhubiri Raia wa Uganda Richard
Mwangusi akiwa chini ya ulinzi wa polisi usiku huu baada ya
kutuhumiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu kupitia huduma ya
M-PESA
Kamanda wa polisi mkoa wa Iringa (RPC) Ramadhan Mungi akitoa kituo cha polisi mjini Iringa ambako mhubiri huyu anashikiliwa na jeshi la polisi kufuatia wananchi kulalamika kufanyiwa vitendo vya kitapeli na mhubiri huyo ,kamanda Mungi amekuwa ni mmoja kati ya makamanda wa mfano nchini kutoka na kufanya kazi usiku na mchana na kuwa jirani zaidi na askari wake
Kikosi cha kazi cha jeshi la polisi mkoa wa Iringa wakiwa njeya kituo cha polisi ambako mhubiri huyo anashikiliwa usiku huu kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu
KILIO cha wengi kuhusiana na vitendo vya utapeli vinavyofanywa na baadhi ya wahubiri ambao wamekuwa wakijitafutia fedha kupitia injili hapa nchini ,kimeanza kusikilizwa baada ya jeshi la polisi mkoa wa Iringa kumkamata na kumtupa mahabusu mhubiri Richard Mwangusi ambae ni raia wa nchini uganda kwa tuhuma za kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Mapema leo kupitia mitandao mbali mbali ya kijamii baadhi ya wasamaria wema wameeleza kusikitishwa na kito cha utapeli kinachofanywa na mhubiri huyo ambae amekuwa akiishi katika nyumba moja ya kulala wageni ya Wihanzi mjini Iringa kuwa amekuwa akiwataka watu mbali mbali kutuma pesa kwa njia ya M-PESA kuanzia kiasi cha kati ya TSh 10,000 na kuendelea iwapo wanahitaji kupanga muda wa kuongea na mhubiri huyo kupitia simu ya kiganjani .
Baadhi ya wananchi ambao walitoa malalamiko yao leo walidai kuwa mhubiri huyo amekuwa akitumia namba ya simu ya Lodge ya Wihanzi ambayo ni 0262700222 kwa kuwataka watu wenye matatizo kupiga simu kwa namba hiyo na mara baada ya kupiga simu mhudumu ambaye yupo zamu amekuwa akimtaka mtu aliyepiga simu kueleza shida yake na mara baada ya kueleza iwapo anataka kuongea na mhubiri huyo amekuwa akitaka kurushiwa kwanza kiasi cha Tsh 10,000 na kuendelea kwa namba ya mhubiri huyo ndipo apewe huduma anayotaka.
Mmoja kati ya watu ambao wamepata kulizwa na mhubiri huyo amedokeza kuwa namba za mhubiri huyo amezipata kupitia kituo kimoja cha Radio mjini Iringa na kutokana na baadhi ya watu kutoa ushuhuda kuwa wamepona magonjwa sugu ndio sababu ya kuchukua namba yake ili kuweza kuombewa pia ila baada ya kuchukua namba hiyo amejikuta akiishia kuliwa pesa bila kupewa huduma husika .
Pia alisema kila anapomtafuta mhubiri huyo kwa njia ya simu ili kuombewa amekuwa akimtaka kuongeza pesa zaidi ili kuombewa hadi kupona jambo ambalo amekuwa akijiuliza kama kwa sasa injili ya biashara na kama biashara basi ni vema wahubiri kutoangaza bei kamili ili mtu apata kununua kulingana na uwezo wake.
Hata hivyo kufuatia kuwepo kwa malamamiko hayo mtandao huu wa www.francisgodwin.blogspot.com na www.matukiodaima.com leo ulipata kupiga simu hiyo majira ya saa 10 jioni na kuomba kuongea na mhubiri huyo ambapo simu hiyo ilipokelewa na mhudumu ya Wihanzi na kudai kuwa kwa wakati huo mhubiri anatoa huduma kwa wateja wengine hivyo ili kuweza kupewa maelekezo ni vema kuwasiliana nae kesho majira ya saa 4 asubuhi.
Kikosi cha jeshi la polisi mkoa wa Iringa chini ya kamanda Ramadhan Mungi na watenda kazi wengine akiwemo OCD ,ofisa upelelezi wilaya na wengine usiku wa leo wameamua kuingia kazini na kupata kumtia nguvuni mhubiri huyo ambae hata hivyo maelezo yake bado yanatia shaka.
Mhubiri huyo anadai kuwa yeye ni Raia wa Uganda na ni mchungaji wa kanisa la I.M na amepata kuifanya huduma kama hii ya mjini Iringa katika nchi kama Zambia , Botswana na nyingine nyingi na katika Tanzania amepata kuzunguka maeneo mbali mbali japo kwa sasa ana zaidi ya miezi miwili katika mji wa Iringa akiishi katika nyumbaya kulala wageni ya Wihanzi .
Kamanda wa polisi mkoa wa Iringa Ramadhan Mungi ameuthibitishia mtandao huu wa www.francisgodwin.blogspot.com kukamatwa kwa mhubiri huyo na kuwa bado jeshi la polisi linaendelea kufanya uchunguzi wa kina ili kujua ukubwa wa madhara ambayo yamessababishwa na mhubiri huyo kwa wananchi na kuwataka wananchi ambao wamepata kuingizwa mjini na mtu huyo kufika kituo cha polisi na kutoa ushirikiano kabla ya mtuhumiwa kufikishwa mahakamani.
Mtandao huu unalipongeza jeshi la polisi mkoa wa Iringa kwa hatua nzuri iliyochukua kuanza kukabiliana na wimbi la wahubiri wasio waaminifu ambao wanaendelea kuchukua fedha kidogo za madafu ambazo wananchi maskini wanazo kwa kisingizio cha kuwasaidi kutatua matatizo waliyonayo .
No comments:
Post a Comment