Pages

Translate

Thursday, 4 July 2013

KUKITHIRI KWA UTOAJI MIMBA NANI ALAUMIWE


Baadhi ya wauguzi na waganga wamelalamikiwa kutokana na kujihusisha na vitendo vya utoaji mimba wasichana.
Wakieleza kusikitishwa kwao kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo, mmoja wa wakazi wa Njoro, Manispaa ya Moshi, Fatma Iddi,  alisema wakati mwingine wazazi wamekuwa ndiyo chanzo cha kuwepo kwa vitendo hivyo kutokana na malezi mabaya wanayotoa kwa watoto wao.

Alisema mzazi anatakiwa kuwa mstari wa kwanza  kuhakikisha mtoto wake wa kike anaishi katika misingi na maadili mazuri na siyo kumuacha akizurura ovyo na wakati mwingine kujihusisha na makundi yasiyofaa.

“Wazazi na walezi kwa kushirikiana na wauguzi ndiyo chanzo kikubwa cha kuwepo kwa vitendo vya utoaji mimba…wauguzi wanapaswa kutoa taarifa polisi juu ya mzazi au msichana atakayefika kwake kwa lengo la kutoa mimba” alisema Fatma.

 Aidha aliwataka wauguzi na wazazi kutoshiriki katika vitendo hivyo vya utoaji mimba  na kufahamu kuwa utoaji mimba ni hatari na ni kinyume na sheria za nchi na haki za binadamu.

Naye mmoja wa wauguzi katika moja ya hosipitali  mkoani Kilimanjaro ambaye jina linahifadhiwa, alikiri kuwapo kwa vitendo hivyo na kusema kuwa hufanywa katika baadhi ya zahanati  na wakati mwingine katika nyumba za kulala wageni  kwa siri kubwa.

“Wapo waganga ambao hufanya kazi hiyo bila uoga na wakati mwingine hutoa kizazi bila  kumshirikisha muhusika, hali ambayo husababisha matatizo makubwa  baadaye” alisema muuguzi huyo.

Naye, Kamanda wa Polisi Mkoani Kilimnjaro, Robert Boaz,  aliwataka wananchi kutoa taarifa pindi wanapogundua kuwapo kwa hospitali inayofanya vitendo hivyo ili wahusika wakamatwe.

No comments:

Post a Comment