Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi jana alikuwa na wakati
mgumu katika Kongamano la Amani lililoandaliwa na Jumuiya ya Wanataaluma
wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udasa), baada ya Katibu Mkuu wa
Chadema, Dk Willbroad Slaa kumtaka ajiuzulu kutokana na kushindwa
kudhibiti uhalifu nchini. Mbali
ya Dk Nchimbi, Mwakilishi wa Mkuu wa Majeshi katika kongamano hilo,
Brigedia Jenerali, Elias Athanas naye alibanwa akitakiwa kueleza tuhuma
za askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kuhusishwa na vitendo
vya ubakaji na utesaji wa raia mjini Mtwara. Akizungumza
katika kongamano hilo, Dk Slaa alisema hakuna haja ya kutafuta mchawi
wa amani ya nchi bali, Serikali inapaswa kulaumiwa kutokana na watendaji
wake kushindwa kuwajibika ipasavyo.
Alitoa
mfano wa kitendo cha Bandari ya Dar es Salaam kutumiwa kupitisha pembe
za ndovu wakati maofisa polisi wakiwemo ni kitendo cha aibu ambacho
kinatosha kumfanya Waziri Nchimbi ajiuzulu. Akijibu
madai hayo wakati akihitimisha kongamano hilo, Waziri Nchimbi alikiri
kuwa baadhi ya polisi wamekuwa na tabia ya kujihusisha na rushwa na
katika kupambana na hali hiyo, Serikali imeshawatimu kazi askari 101
katika kipindi cha mwaka 2012. Hata
hivyo, Dk Nchimbi alisema suluhisho la matatizo yaliyopo ndani ya Jeshi
la Polisi siyo kuwatimua kazi askari pekee na ndiyo maana Serikali
imeanza mkakati wa kutoa mafunzo ya maadili ili kuwawezesha kufanya kazi
zao kwa weledi.
Akijibu
tuhuma hizo, Brigedia Jenerali Athanas alikanusha madai hayo akisema
siyo kweli kwamba JWTZ linaendesha unyama na kwamba lipo Mtwara kwa
ajili ya kulinda amani na kusema tuhuma hizo ni za mitaani. Mbunge
wa Singida Mashariki (Chadema), alidai kuwa tangu nchi ilipopata uhuru
haijawahi kuwa na amani ya kweli akitoa mfano wa wananchi kuhamishwa kwa
nguvu katika maeneo yao. Alisema
katika siku za karibuni, tofauti na zamani polisi ilipokuwa ikifanya
kazi ya kudhibiti uhalifu, sasa inaonekana kama kazi yake ni kudhibiti
upinzani na limekuwa likituhumiwa mara kwa mara kwa kufanya vitendo vya
uvunjifu wa amani na kusababisha mauaji.
Alipiga kijembe akisema kwamba CCM kinakaribia kuanguka na ndiyo maana kimekuwa kikitumia mabavu kudhibiti upinzani. Awali,
Profesa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Gaudence Mpangala alisema
amani inaweza kutoweka ikiwa CCM kitaendelea kutumia dola kudhibiti
upinzani. Alisema
CCM kinapaswa kufanya kazi kama ilivyo vyama vingine vya siasa na
kuonya kwamba hata kukiwa na makongamano mengi, amani haitapatikana kama
hakitajitathmini na kuchukua hatua. Alisema
polisi imekuwa ikifanya makosa kuzuia maandamano ya vyama vya upinzani
akisema sheria iko wazi ikisema vinachotakiwa kufanya ni kulitaarifu
jeshi hilo kuhusu ratiba ya shughuli zake.
No comments:
Post a Comment