ASEMA SMG, BASTOLA ZILITUMIKA ARUSHA
MWENYEKITI wa CHADEMA Freeman Mbowe, amevituhumu vyombo vya dola kuwa vinawafahamu watu walioshiriki kwenye mlipuko wa bomu uliotokea jana katika viwanja vya Soweto kwenye mkutano wa chama hicho.
Mbowe, alisema tukio hilo ni la kupangwa na wamegundua risasi za bunduki aina ya SMG na bastola zilitumika mara baada ya mlipuko huo jambo linalozusha hofu na kudidimiza demokrasia ya vyama vingi.
Wakati Mbowe akitoa tuhuma hizo kwa vyombo vya dola, Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Said Mwema ameunda timu itakayoongozwa na makamishna wawili (Paul Chagonja na Isaya Mungulu), kwenda mkoani Arusha kuongeza nguvu ya uchunguzi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mkoani hapa, Mbowe alisema uchunguzi wa awali walioufanya wamebaini tukio hilo ni la kisiasa na lilipangwa.
Alisema ni vema serikali ikatangaza kuachana na mfumo wa vyama vingi kuliko kuruhusu mauaji na vurugu katika mikutano ya vyama vya upinzani vinavyoonekana kutoa wakati mgumu kwa watawala.
Aliongeza kuwa uchunguzi wa awali katika eneo la tukio umebaini bomu lililolipuliwa ni la kiwandani na si la kutengenezwa.
Alisema katika eneo la tukio maganda ya risasi kutoka katika bunduki ya SMG na bastola yalikutwa hali inayowafanya waamini kuna watu waliamua kufanya tukio hilo kwa kupanga.
Mbowe alisema risasi hizo pia ni miongoni mwa zilizopigwa kwenye tanki la mafuta la gari la matangazo la CHADEMA ambapo zililitoboa.
Alibainisha kuwa inavyoonekana wahusika walitaka kuzalisha mlipuko mwingine mkubwa na kuleta maafa makubwa katika mkutano huo.
“Haihitaji uchunguzi wa kwenda mwezini katika suala hili, ni wazi walipanga kutuua lakini wakaua watu wasiohusika. Waliouawa hawakuwa katika mpango wao na wamekuwa wahanga kwa niaba yetu.
“Hata kama utaamua kumuua Mbowe au (Godbless) Lema, huwezi kuiua CHADEMA kwani chama kitabaki, na wanachama wengine wataendeleza harakati za chama kama kawaida,” alisema.
Wabunge kutohudhuria Bunge
Mbowe alisema kutokana na tukio hilo ambalo limeua watu zaidi ya watatu, CHADEMA imeamua kulifanya ni la kitaifa na wabunge wake watashiriki kwenye maombolezo.
Alisema kuanzia leo wabunge wote wa CHADEMA hawatahudhuria vikao vya Bunge na watajumuika mkoani Arusha hadi misiba yote itakapomalizika.
Alisema wanatarajia kufunga mahema katika eneo la tukio na marehemu wote wataagwa katika eneo hilo ambapo ibada zote za Kiislamu na Kikristu zitafanyikia hapo.
IGP aunda timu
Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mwema ameunda timu ya kuongeza nguvu ya uchunguzi itakayoongozwa na makamishna wawili ambao ni Paul Chagonja kutoka idara ya operesheni na Isaya Mngulu kutoka ofisi ya upelelezi makao makuu.
IGP Mwema alisema baada ya tukio hilo, jeshi hilo lilituma makamishna wawili kutoka makao makuu kwa ajili ya kuongeza nguvu ya uchunguzi wa tukio hilo na kwamba wameshaanza kukusanya taarifa mbalimbali zitakazoweza kusaidia kuwabaini watu waliohusika.
Alisema wameunganisha nguvu na vyombo vingine vya ulinzi na watawasaka wahalifu hao pamoja na walio nyuma yao kwa kile alichoeleza tukio hilo linaashiria kushamiri kwa matendo ya kigaidi nchini.
Akizungumzia tuhuma zinazotolewa na wananchi juu ya Jeshi la Polisi kuwajeruhi watu kwa risasi za moto, IGP Mwema alisema kila taarifa inafanyiwa kazi kwa umakini na kwamba baada ya uchunguzi watatoa taarifa kamili kwa umma juu ya kilichotokea jijini Arusha.
Aliwaomba wananchi wenye taarifa za kuweza kumtambua aliyerusha bomu pamoja na watu walio nyuma yake wajitokeze au wamtumie ujumbe kupitia simu yake ya mkononi namba 0754 78 55 57 na kwamba uhusika wao utafanywa kuwa siri.
IGP Mwema pia alisema watachunguza kauli ya Naibu Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) bara, Mwigulu Nchemba aliyowaambia wakazi wa Kimandolu kuwa wasipoichagua CCM katika uchaguzi wa madiwani wa Jiji la Arusha ulioahirishwa jana, watakufa.
Mwema alisema watachunguza kauli hiyo baada ya kuulizwa swali la hatua zilichochukuliwa kabla na baada ya mlipuko huo dhidi ya kauli ya Nchemba.
Juzi katika mkutano wa kufunga kampeni za udiwani kwa CHADEMA uliofanyika kwenye viwanja vya Soweto, kitu kinachodhaniwa ni bomu kilipuka na kuua watu watatu na wengine kujeruhiwa.
chanzo:Chadema blog
No comments:
Post a Comment