Pages

Translate

Tuesday, 25 June 2013

MTU MMOJA AUAWA KISA MZOZO WA MASHAMBA



Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya Diwani Athumani
MKOA wa Mbeya ukiwa ni moja ya mikoa inayoongoza kwa migogoro na kesi za ardhi, imefikia hatua sasa wananchi wameanza kuviziana na kuuana.
Mkulima wa Kijiji cha Suma wilayani Rungwe Saita Mboma(65), amefariki dunia baada ya kuvamiwa usiku nyumbani kwake na kukatwakatwa na mapanga.
Taarifa ya Jeshi la polisi mkoa wa Mbeya iliyosambazwa kwenye vyombo vya habari leo na kusainiwa na kamanda wa polisi Diwani Athumani, imesema tukio hilo lilitokea Juni 22, mwaka huu kijijini hapo na kukutwa na mauti Juni 24, mwaka huu.
‘Kabla hajapatwa na mauti alikimbizwa katika hospitali ya Makandana wilayani humo kwa ajili ya matibabu ambapo taarifa zinasema kuwa alikuwa akiishi peke yake na alivamiwa akiwa amelala na chanzo ni mzozo wa muda mrefu wa mashamba’’ imeeleza taarifa hiyo.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa watuhumiwa wa tukio hilo wamekamatwa ambao ni Salum Mwambona(45) na Feda Busila ambao wote ni wakazi wa kijiji cha Itagata na taratibu za kuwafikisha mahakamani zinafanywa.
Wakati huo huo, ajali za barabarani zimegeuka janga la mkoa wa Mbeya ambapo hazipiti siku Nne bila kupoteza maisha ya watanzania au kupata ulemavu wa kudumu.
Katika mwendelezo wa ajali hizo, askari Polisi wa kikosi cha FFU Jijini Mbeya, amefariki papo hapo baada ya kugongwa na gari eneo ya barabara ya Benki kuu Jijini hapa.
Taarifa polisi, imesema kuwa  ajali hiyo ilitokea Juni 23 mwaka huu.
Taarifa hiyo imesema kuwa gari na dereva asiyefahamika, liligonga gari T.741 BXU aina ya March lililokuwa limeegeshwa eneo la hilo kisha kumgonga mtembea kwa miguu askari Polisi aitwaye  EX.G 9386 PC Patrick(23) na kusababisha kifo chake papo hapo.
‘’Chanzo kinachunguzwa. Dereva alikimbia na gari mara baada ya tukio na mwili wa marehemu umesafirishwa kwenda Dodoma kwa ajili ya mazishi na yeyote mwenye taarifa za alipo dereva huyo na gari atoe taarifa kwenye mamlaka husika ili sheria iweze kuchukua mkondo wake’’ imesema taarifa hiyo.
Mbali na ajali hiyo, jana Juni 25, mwaka huu, ajali nyingine imesababisha kifo cha Vedasto Emmanuel(20) na majeruhi kwa watu watano eneo la Njia panda Ilomba Jijini Mbeya.
Watu waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni Lusajo John(22), Yohana Daud(20), Hussein Mbilinyi(20), ambao wamelazwa hospitali ya rufaa ya Mbeya na mwingine ni Andrew Daud(20).

No comments:

Post a Comment